KCSE Kiswahili Paper 2 2010

Find KCSE Kiswahili Paper 2 2010. Kenya Certificate of Secondary Education Kiswahili Paper 2 Past paper

 

1. UFAHAMU  (ALAMA 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali

Suala la mahusiano ya wanadamu katika jamii, uainishaji wake na udhihirikaji wake  limewashughulisha wataalamu wa elimu jamii kwa dahari ya miaka. Suala hili  huwatafakarisha wataalamu hao kutokana na umuhimu wake katika maisha ya binadamu,  Msingi mkuu wa uainishaji wa mahusiano hayo ni kukichuza kipindi cha mahusiano  yenyewe. Yapo mahusiano baina ya waja ambayo yanachukua muda mfupi, kwa mfano saa  au dakika chache, na mengine ambayo huenda yakachukua miaka ayami.

Mahusiano ya muda mrefu kabisa ni yale yanayojulikana kama mahusiano ya kudumu.  Inamkinika kudai kuwa miundo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi huweza kuyadhibiti  mahusiano hayo kwa kiasi kikubwa. Watu wengi huitakidi kuwa uhusiano uliopo baina ya  mtu na jamaa yake utachukua muda mrefu, na kwa hivyo ni uhusiano wa kudumu. Hali hii  hutokana na uhalisi kuwa tunahusiana na jamaa zetu kwa kipindi kirefu labda tangu ukembe  hadi utu uzima wetu. Uhusiano huu hautarajiwi kuvunjwa na umbali wa masafa baina yetu;  tunaendelea kuwasiliana kwa barua au, katika enzi hii ya utandawazi, kwa kutumia nyenzo  za teknohama kama mtandao na simu za mkononi, na kudumisha uhusiano wetu wa kijamii.  Hata hivyo, inawezekana baadhi ya mahusiano ya kijamii yasiwe ya kudumu. Mathalan,  uhusiano uiiopo baina ya mke na mume, na ambao unatarajiwa kuwa wa kudumu au wa  kipindi kirefu, unaweza kuvunjwa kwa kutokea kwa talaka. Talaka hiyo inavunja ule  uwezekano wa uhusiano wa kudumu unaifumbatwa na sitiari ya pingu za maisha.

Katika ngazi ya pili, mahusiano ya kipindi cha wastani, kuna mahusiano yanayouhusisha  marafiki zetu maishani, shuleni au kwenye taasisi zozote zile, majirani zetu. wenzetu katika  mwahali mwa kazi, washiriki kwenye sehemu za ibada au za burudani na wenzotu kwenye  vyama tofauti na makunci ya kujitolea. Inawezekana kudahili kuwa baadhi ya mahusiano  haya, hususan baina ya marafiki na majirani huweza kuwa ya miongo na daima. Hali hii  huweza kutegemea muundo na mfumo wa jamii. Kwa mfano, kwa wanajamii wanaoishi  kwenye janibu Fulani mahsusi, na kwa miaka tawili bila ya kuhajiri, uhusiano wao na  majirani huweza kuwa wa kudumu. Hali hii inasigana na hali iliyoko kwenye maisha ya mjini.  Maisha ya mijini yana sifa ya kubadilikabadilika. Isitoshe, kutokana na mfumo wa maisha ya  kibepari yameghoshi ubinafsi mwingi. Mawimbi ya mabadiliko na ubinafsi huweza  kuumomonyoa ukuta wa uhusiano wa kudumu.

Mwelekeo wa maisha ya siku hizi ya uhamaji kutoka maeneo au viambo walikoishi watu  unasababisha kupombojea kwa mahusiano ya kudumu baina yao na majirani zao. Uhusiano  kati ya wenza katika mazingira ya kazi unahusiana kwa kiasi Fulani na ule wa majirani.  Vimbunga vya ufutwaji kazi, ubadiishaji wa kazi, hali zisizotegemewa na mifumo ya  kimataifa pamoja na hata mifumo ya kisiasa huweza kuathiri mshikamano wa wanaohusika  kazini.

Kiwango cha mwisho cha mahusiano ni uhusiano wa mpito au wa muda mfupi. Mahusiano ya aina hii hujiri katika muktadha ambapo pana huduma Fulani. Huduma hizi zinaweza kuwa za dukani, kwenye sehemu za ibada, kwenye kituo cha mafuta, kwa kinyozi, kwa msusi na kakdhalika. Kuna sababu kadha zinazotufanya kuyazungumzia mahusiano ya aina hii kama ya mpito. Kwanza, uwezekano wa mabadilkio ya anayeitoa huduma hiyo ni mkubwa. Si ajabu kuwa unaporudi kwa kinyozi au msusi unatambua aliyekushughulikia hayupo. Hata hivyo, kuna vighairi hususan pale ambapo mtoa huduma anayehusika ni yule yule mmoja.

Mahusiano ya mpito yanatawaliwa na ‘uhusiano wa chembe chembe.’ Uhusiano wa chembe chembe, bidhaa ya mfumo wa kibepari, unamaanisha kuwa kinachomshughulisha mtu ni chembe ndogo tu ya mwenzake. Chembe hiyo inaweza kuwa huduma, kwa mfano, gazeti analokuuzia mtu, viatu anavyokushonea, nguo anazokufulia, ususi anaokufanyia n.k. Mahusiano ya aina hii yametovukwa na hisia za utu na ni zao !a mifumo ya kisiasa ya kiuchumi na kijamii. Mtu anayehusiana na mwenzake kwa misingi ya chembe ndogo tu, huenda asijali kama mwenzake amekosa chakula, amefutwa kazi, amefiiiwa, ameibiwa na kadhalika.

Suala kuu tunalopaswa kujiuliza ni: je, tunahusiana vipi na jamaa zetu, marafiki zetu na majirani zetu? Je, uhusiano wetu na raia wenzetu ni wa aina gani? Je, uhusiano wetu na nchi yetu ni wa mpito au ni wa kudumu?

   (a) Taja kigezo muhimu cha kuzungumzia mahusiano.           (alama 1)

   (b) Eleza imani ya watu kuhusu uhusiano baina ya jamaa.        (alama 1)

   (c) Fafanua athari ya teknolojia kwenye mahusiano ya watu.       (alama 2)

   (d) Eleza sababu nne kuu za kuharibika kwa mahusiano katika maisha ya leo.    (alama 4)

   (e) Taja sifa kuu ya mahusiano ya muda mfupi.    (alama 2)

    (f) Je, kifungu hiki kina ujumbe gani mkuu?     (alama 2)

   (g) Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa katika kifungu.      (alama 3)

         (i) inasigana

         (ii) yameghoshi

         (iii) vighairi

 

2.  MUHTASARI  (ALAMA 15)

Jamii ya leo inatawaliwa na kuendeshwa na kanuni ya maarifa. Inawezekana kusema kuwa uchumi wa jamii za leo na zijazo utategemea maarifa zaidi kuliko utakavyotegemey uwezo wowote mwingine. Utambuzi wa uwezo mkubwa wa maarifa katika maisha ya binadamu ndio msingi wa watu kusema ‘maarifa ni nguvu.’

Maarifa huelezwa kwa tamathali hii kutokana na uwezo wa: kuyadhibiti. kuyaendesha, kuyatawala na kuyaongoza maisha ya binadamu popote pale walipo. Mtu ambaye ameyakosa maarifa fulani huwa ameikosa nguvu hiyo muhimu na maisha yake huathirika pakubwa. Kwa msingi huu, maarifa yanaweza kuangaliwa kama utajiri mkubwa ambao binadamu anaweza kuutumia kwa faida yake au kwa faida ya wanajamii wenzake. Ukweli huu ndio unaoelezwa na methali ya Kiswahili: ‘Elimu ni mali’Elimu ni chimbuko la maarifa muhimu maishani.

Msingi wa utajiri na maendeleo ya binadamu popote alipo basi ni maarifa. Je, marifa kwa upande wake yana sifa gani? Maarifa yenyewe hayana upinzani. Maarifa uliyo nayo huweza kuwa na watu wengine wengi pasiwe na upinzani baina yenu kwa kuwa kila mmoja ana maarifa sawa. Kila mmoja ana uhuru wa kuyatumia maarifa hayo kama chanzo cha kuyazalisha maarifa mengine. Utumiaji wa maarifa yenyewe hauyamalizi maarifa hayo. Maarifa hayawezi kugusika ingawa mtu anaweza kuyanyumbua maarifa yenyewe kwa kuyatumia kwa namna tofauti.

Maarifa huingiliana na maarifa mengine. Maarifa aliyonayo mtu mmoja huweza kuhusishwa na maarifa aliyo nayo mtu mwingine ili kuvyaza au kuzuka na maarifa tofauti. Maanfa yanaweza kuchukuliwa kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa namna ambavyo mtu hawezi kufanya bidhaa nyingine ile. Kwa mfano, ni muhali mtu kulalamika kuwa hawezi kutembea kutoka sehemu rnoja hadi nyingine kwa sababu ana mzigo mzito wa maarifa kichwani.

Sifa nyingine muhimu ya maarifa ni kuwa yanaweza kuwasilishwa kwa njia za ishara au mitindo mingine ya kidhahania. Ikiwa unataka kukihamisha chombo Fulani kutoka sehemu moja hadi nyingine, lazima uwazie ukubwa wake, uzito wake na labda hata umbal.i wa panapohusika. Maarifa huweza kubadilishwa au kugeuzwa na kuwa ishara ambazo huyafanya kuwasilishwa kwa njia nyepesi kuliko kwa mfano ikiwa mtu atayawasilisha katika muundo wa, kwa mfano, kitabu.

Maarifa yana sifa ya uhusianaji. Kipengele Fulani cha maarifa huwa na maana kinapowekwa sambamba au kugotanishwa na kipengele kingine cha maarifa. Huo huwa muktad’na mzuri wa kueleweka au kuwa na maana. Kw amfano, neno ‘mwerevu’huweza kuwa na inaana kwa kuwekwa katika muktadha wa ‘mjinga”mjanja’, ‘hodari’na kadhalika.

Maarifa huweza kuhifadhiwa katika nafasi ndogo sana. Suala hili linaeleweka kwa njia nyepesi tunapoangalia maarifa katika muktadha wa teknologia. Data zinazowahusu mamilioni ya watu, ambazo zingehitaji maelfu ya maktaba na lukuki ya vitabu, huweza kuhifadhiwa kwenye kifaa kidogo kinachoweza kutiwa mfukoni.

Maarifa hayawezi kudhibitiwa au kuzuiliwa mahali fulani yasisambae. Maarifa hucnea haraka sana. Maarifa ni kitu kinachoepuka pingu za watu wanaopenda kuwadhibiti binadamu wenzao. Hata pale ambapo mfumo wa kijamii au wa kisiasa unafanya juu chini kuwadhibiti raia au watu wenyewe, ni muhali kuyadhibiti maarita yenyewe. Inawezekana kuzidhibiti njia Fulani za ueneaji wa maarifa lakini maarifa hayo yatapata upenyu wa kusambaa. Ni kweli kuwa maarifa ni nguvu inayozishinda nguvu zote.

(a) Fupisha aya ya pili na ya tatu. (maneno 55 – 60)      (alama 5, 1 ya utiririko)   Matayarisho,  Nakala Safi

(b) Eleza sifa kuu za maarifa kama zinavyojitokeza kuanzia aya ya nne hadi aya ya nane. (maneno 100 -110)      (alama 10, 2 za utiririko) Matayarisho Nakala Safi

 

3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)

(a) Toa mfano wa neno lenye muundo wa silabi ya irabu pekee.     (alama 1)

(b) Eleza maana mbili za neno: Barabara.     (alama 2)

(c) Sahihisha sentensi:

       Abiria walisafiri na ndege.      (alama 1)

(d) Tambua na ueleze aina za vivumishi katika sentensi:

        Mwanafunzi mkongwe amcpewa tuzo kwa kuwa hodari masomoni.     (alama 4)

 

(e) Andika sentensi ifuatayo katika hali yakinishi.

       Usingeacha masomo, usingetaabika vile.       (alama 2)

(f) Tunga sentensi ukitumia kielezi cha:

          (i) Jumla              (alama 1)

          (ii) Namna linganisho   (alama 1)

(g) Ainisha shamirisho na chagizo katika sentensi:

        Vibarua wamefanya kazi haraka ipasavyo.   (alama 2)

(h) Eleza maana mbili zinazopatikana katika sentensi:

      Nenda ukaniletee mbuzi.    (alama 2

(i) Tunga sentens kudhihirisha matumizi ya ngeli ya U-U.     (alama 2)

(j) Andika katika usemi wa taarifa.

“Mito yetu imechafuka sana; itabidi tuungane mikono wakubwa kwa wadogo, wanaume kwa wanawake ili tuisafishe.” Mwanamazingira alituhimiza.   (alama 3)

(k) Changanua sentensi ifuatayo ukitumia mistari au mishale.

          Amina na Mustafa huimba taarabu.   (alama 4)

(I) Eleza matumizi ya ku katika sentensi:

        Sikumwelewa alivyoeleza namna ya kuwatunza mbwa wake.     (alama 2)

(m) Tunga sentensi sahihi ukitumia kitenzi la katika kauli ya kutendwa.     (alama 2)

(n) Eleza kazi ya kila kitenzi katika sentensi:

 

          Mkulima angetaka kupalilia shamba lake mapema.      (alama 4)

(o) Taja na utofautishe vipasuo vya ufizi.     (alama 4)

(p) Onyesha jinsi moja moJa ya matumizi ya viwakifishi vifuatavyo:)

          (i) Nusu koloni (;)     (alama 1)

           (ii) Herufi kubwa     (alama 1)

           (iii) Kishangao (!)     (alama 1)

 

 4. ISIMUJAMII  (ALAMA 10)

“Benki yenyewe haina kitu…CD4 count yake iko chini.-Ni emergency…Tutampoteza ikikosekana.”

   (a) Taja sajili inayorejelewa na maneno haya.     (alama 2)

   

   (b) Fafanua sifa nne zinazoh’usishwa na sajili hiyo.      (alama 8)